Jumatano, 26 Oktoba 2016

JIFUNZE ASILI YA WACHAGA NA DESTURI YAO

WACHAGA ni kabila la kibantu linalopatikana Kaskazini mwa Tanzania katika mkoa wa Kilimanjaro.

Wachaga wanajishughulisha na kilimo cha viazi, ndizi na mtama. Zao la kahawa lilianzishwa na wakoloni karne ya 19 na kuendelezwa hadi leo kama zao la biashara. Pia wachagga hujihusisha na ufugaji wa ng'ombe, mbuzi na kondoo ili kupata samadi ya kurutubisha mashamba, nyama, maziwa.

Miaka ya nyuma ufugaji wa mbuzi au kondoo ulikuwa wa lazima ili kupata wanyama wa kutambika. Ilikuwa ni mwiko kutambika kwa kutumia mnyama wa kununua au kutoka nyumba nyingine. Kutokana na uhaba wa ardhi katika makao yao ya asili, Wachaga wametawanyika sehemu mbalimbali ndani na nje ya nchi wakijishughulisha na kazi mbalimbali ili kupambana na umasikini.

Ingawa baadhi ya hadithi za kale zinaeleza kuwa Wachaga walikuwepo eneo la Kilimanjaro na dua zao ndizo zilizorefusha mlima Kilimanjaro ili waweze kuwa karibu na Mungu, utafiti unaonesha kuwa Wachaga ni wahamiaji waliofika Kilimanjaro miaka 600 kabla ya ujio wa Kristo. Hivi sasa ni zaidi ya miaka 2000 baada ya Kristo.

Tafiti kuhusu makabila zinasema endapo Wachaga wataamua kutafuta asili yao kwa kuzingatia kizazi cha kale ni lazima wabishe hodi kwenye jamii za makabila mbalimbali hasa kwa Wakamba, Wamaasai na Wataita nchini Kenya, pia kwa Wapare, Wasambaa nchini Tanzania.

Tofauti na makabila mengine ambayo asili yao inatokana na kizazi kimoja, Wachaga wanaweza kujua asili ya kizazi chao kwa kufuatilia historia ya ukoo au historia ya makundi kulingana na eneo. Historia ya kale inasema kuwa jamii ya wachaga inatokana na watu wa makabila mbalimbali ambao walihamia kwenye mteremko wa mlima Kilimanjaro baada ya kukimbia vita na wengine kukimbia baa la njaa.

Pia wapo waliohamia eneo hilo baada ya kuvutiwa na ardhi yenye rutuba na hali nzuri ya hewa na inasemekana kuwa wahamiaji hao waliwazidi nguvu wenyeji wa eneo hilo ambao walijulikana kama Koningo au Konyingo. Baadhi ya wenyeji walihama ila inasemekana kuwa wengine walibaki na kujumuika na wahamiaji na baada ya kuishi pamoja kwa muda mrefu waliunda kabila jipya la wachaga.

Ingawa hakuna ushahidi wa kisayansi kuwa Wachaga walitokana na makabila mengine, simulizi za kale na mfumo wao wa maisha unadhihirisha kuwa hawatokani na kizazi kimoja wala wazee na viongozi wao hawajawahi kuwa na uhusiano wa karibu.

Ingawa watu hao huitwa wachaga wenyewe ni vigumu kujua nani hasa ni Mchaga kwa kuwa wenyeji hutambuana kwa kutumia lugha ya eneo husika kama vile
Mrombo,
Mmachame,
Muuru,
Mkibosho au Muanjo akimaanisha mchaga wa Marangu. Uongozi wa jamii ya Wachaga ulitumia mfumo wa machifu, maarufu kama Mangi.

Kila eneo lilikuwa na mangi wake, ila Mangi Sina wa Kibosho, Rindi wa Moshi na Marealle wa Marangu walipata umaarufu mkubwa, kutokana na jitihada zao za kutaka kuwa wafalme ili kutawala himaya nzima ya wachaga. Hata hivyo, jitihada hizo ziligonga mwamba kwa kuwa hakuna Mangi aliyekuwa tayari kutawaliwa na kiongozi kutoka kundi jingine.

Hali ya kujihami na kuogopana inachukuliwa kama kielelezo kuwa chimbuko la wachaga linatokana na jamii za makabila tofauti yenye historia tofauti.

Mfumo wa uongozi miongoni mwa wachaga umeathiri kizazi kipya kwa kuwa uzoefu unaonesha kuwa wachaga ni miongoni mwa jamii chache zinazopenda siasa za upinzani na hupenda kuchagua kiongozi kwa kupima uwezo wa mtu badala ya chama.

Kati ya mwaka 1750 na mwaka 1890 Wachaga walikuwa na vita vya mara kwa mara, ambapo kila Mangi alitaka kutwaa eneo la mwenzake ili kuongeza ukubwa wa ardhi na kuimarisha ngome yake kiuchumi.

Hadi Mwanzoni mwa Karne ya 19 , wachaga waligawanyika katika makundi 30 na kila kundi lilikuwa na Mangi wake na walijitegemea mithili ya nchi 30 katika kisiwa kidogo chenye udongo wenye rutuba, hali ya hewa safi na chemchemi za maji kila baada ya hatua chache.

Wachaga walikuwa na bendera yao na siku maalumu ya mapumziko, maarufu kama Siku ya Wachaga, ambapo watu walikutana kwa ajili ya kula na kucheza pamoja ili kuimarisha mshikamano upendo na mshikamano. Makundi hayo yalizungumza lugha tofauti na lahaja tofauti, kulingana na jiografia ya eneo husika.

Watu hao waliwindana kila mmoja akimnyooshea mwenzake kidole kwa uchokozi na tamaa ya kutwaa mali na ardhi ya kundi jingine. Vita vya wachaga viliimarika baada ya kuingia kwa Wamisionari, ambao walifika Kilimanjaro na kueneza dini ya Kikristo pamoja na kuanzisha zao la kahawa.

Hivyo, machifu waliweka silaha chini na kuelekeza nguvu zao kwenye kilimo cha kahawa. Wakoloni walifurahi hali ya utengano miongoni mwa Wachaga hivyo walitumia fursa hiyo kuwalaghai machifu ili waweze kupata ardhi kubwa na rasilimali nyingi. Kila chifu alijitahidi kuwakarimu wageni ili aweze kupata msaada wa kujiimarisha kiuchumi na kisiasa.

Kwa mujibu wa historia ya Wachaga, iliyoandikwa na Stanl Kathleem mwaka 1962, kabila hilo lilikuwa na viongozi wengi, ila wachache walipata umaarufu kutokana na aina ya uongozi wao.

Mwaka 1800 chifu aliyejulikana kama Mangi Horombo kutoka Mashariki mwa mlima Kilimanjaro, alikuwa na nguvu zaidi na aliweza kutwaa maeneo yaliyokuwa na wachaga wasiokuwa na nguvu kiuchumi wala kisiasa.

Hata hivyo baada ya kifo cha Horombo himaya yake iligawanyika na kuunda vikundi vidogo vinavyojitegemea. Wakati Muingereza wa kwanza, Johannes Rebmann, alipofika Kilimanjaro mwaka 1848 alikuta mangi wa Machame na Mangi wa Kilema wakiwa na nguvu kubwa kisiasa na kiuchumi, lakini alififia kutokana na sababu mbalimbali.

Kathleem anasema Mangi Oromba alikuwa kiongozi jasiri katika eneo la Mashariki mwa Mlima Kilimanjaro na aliogopwa na watu wake kwa kuwa alikuwa mtu mwenye msimamo. Kiongozi huyo aliishi eneo ambalo hivi sasa linafahamika kama wilaya ya Rombo. Alikuwa Mangi wa kwanza kuanzisha wazo la kujenga himaya ya Wachaga.

Alijenga ngome yake katika kijiji cha Keni na kuunja jeshi, ambalo lilivamia himaya za machifu wengine na kufanikiwa kuteka eneo la Vunjo hadi mto Nanga. Hata hivyo, baada ya kifo chake himaya yake iligawanyika na kurudi katika vikundi vidogo vidogo kwa kizingatia asili na chimbuko la kila kikundi.

Mangi Sina alikuwa jasiri kama Orombo na aliyongoza himaya ili- yokuwa Magharibi mwa mlima Kilimanjaro hadi mpakani kwenye mto Nanga. Alijenga ngome yake katika eneo la Kibosho, ila alitawala hadi eneo la Marangu na Uru. Mwaka 1870 alijenga mji wa kibiashara kati ya Waafrika na Waarabu, ambapo waarabu walimpa nguo na silaha kisha akatoa pembe za ndovu vitu vingine vya thamani.

Utawala wa Mangi Sina ulififia mwaka 1891 wakati waingereza walipoamua kumuongezea nguvu Mangi Rindi wa Moshi, kisha kumtumia kudidimiza utawala wa Mangi Sina. Mangi Rindi ambaye alijulikana kwa jina la Mandara, alikuwa kiongozi wa Moshi mwaka 1860. Alikuwa miongoni mwa viongozi waliokuwa na ndoto ya kutawala eneo lote la Kilimanjaro.

Ili kufanikisha mikakati yake aliungana na viongozi wa kabila la Arusha eneo la mlima Meru na waswahili kutoka Pwani, kisha kusaini mkataba wa Wajerumani kwa lengo la kuiweka Kilimanjaro chini ya Utawala wa kijerumani katika Ukanda wa Afrika Mashariki.

Mwaka 1891 alifanikiwa kuhifadhi ngome ya kijeshi ya Wajerumani kwa ajili ya kusambaratisha utawala wa Mangi Sina wa Kibosho. Uhusiano wa Mangi Rindi na Wajerumani, uliwezesha Moshi kuwa makao makuu ya mkoa wa Kilimanjaro hadi mwaka 1919 wakati makao ya mji huo yalipohamishiwa eneo la kudumu ulipo mji wa Moshi hivi sasa.

Mangi Marealle wa Marangu alisimikwa na Mangi Sina mwaka 1880 wakati eneo la Marangu lilipokuwa sehemu ya himaya ya Kibosho.

Mangi Marialle wa kwanza alikuwa kijana mwerevu na mwenye shauku ya kuwa kiongozi bora kuliko waliomtangulia Kwa kuwa Mangi Marealle hakuwa mtu wa kutumia mitutu, aliamua kujifunza lugha ya kigeni ili kuweza kuwasiliana moja kwa moja na viongozi wa Kiarabu na wakoloni wa Kiingereza na kuwaalika kuwekeza katika eneo la Marangu.

Pia, alijaribu kujenga urafiki na uongozi wa utawala wa Kijerumani na inadaiwa inadaiwa kuwa 1890 Mangi Marealle alifanikiwa kushawishi uongozi wa jeshi la Kijerumani, kuamini kuwa kuwa watu wa kibosho na Moshi walikuwa na njama ya kuangusha kutawala wa Kijerumani, jambo ambalo lilisababisha machifu wa Kibosho na Moshi kunyongwa na utawala wa Kijerumani.

Himaya ya Watu wa Machame ilijengwa na Mangi Abdiel Shangali, ambaye aliingia madarakani mwaka 1923 na kuongoza mfululizo hadi mwaka 1946 alipopandishwa cheo na kuwa chifu wa jimbo la Hai, kwa kujumuisha eneo la Machame na kibosho.

Mangi Shangali alitawala kipindi cha amani, hivyo alifanikiwa kubadilisha mfumo wa uongozi kutoka utawala wa kichifu wa kuridhishana hadi utawala wa mfumo wa kisasa kwa kuchagua viongozi kwa njia ya demokrasia.

Hata hivyo, wachaga hawakuacha kuzozana kuhusu uhaba wa ardhi na hali hiyo iliendelea hadi Tanganyika ilipopata uhuru na kufunja mfumo wa utawala kitemi na kuunda serikali ya umoja wa Kitaifa. Baada ya Uhuru wachaga waliendelea kukodoleana macho kila kundi likitamani ardhi ya kundi jingine.

Hata hivyo Rais Nyerere alifanikiwa kumaliza tatizo hilo kwa kuwahimiza wachagga watawanyike na kushika ardhi katika maeneo mengine katika ardhi ya Tanzania badala ya kung'an'gania ardhi ndogo katika mteremko wa mlima Kilimanjaro.

Hali hiyo iliwafanya Wachaga kuamua kuwekeza katika elimu ili kuwawezesha watoto wao kujenga uwezo wa kujitegemea na kwenda kutafuta maisha sehemu nyingine. Hali hiyo imewawesha wachagga kutawanyika sehemu mbalimbali ndani na nje ya nchi kujitafutia maisha kwa kushiriki katika nyanja mbalimbali hasa katika uongozi wa mashirika, ualimu na biashara.

Watafiti wa masuala la kisiasa wanasema mfumo wa maisha ya Wachaga, umesababisha watu wa kabila hilo kuwa washabiki wa siasa zenye upinzani kutokana na tabia yao ya kujihami kisiasa.

Ingawa viongozi kadhaa wa juu wa vyama vya upinzani wanatoka mkoa wa Kilimanjaro, inaelezwa kuwa ni vigumu viongozi hao kuunganisha vyama vyao na kuunda chama kimoja chenye nguvu, kutokana na ukweli kuwa hata Machifu wa zama za kale, walishindwa kuungana na kuchagua mtawala mmoja.

NB:Kama ilivyo kwa Watanzania wengine, Wachaga wanapokuwa katika mikoa au nchi tofauti, husahau tofauti zao za nyumbani na kushirikiana kama ndugu wa mama mmoja. Hali hiyo imewezesha wachagga kuishi popote na kushirikiana na watu wa makabila mengine bila kusahau utamaduni wa kwenda kwao angalau mara moja kila mwaka.

Naamini umejifunza kitu kipya ama umeongeze ufahamu kuhusu wachaga

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni