Mtu kuweka akiba, ni muhimu sana kama vile ilivyo kwa taifa. Saikolojia ya matumizi ya fedha inaonyesha kuwa mtu hupenda kutumia sasa kuliko kusubiri baadaye ambapo ingeongeza faida na thamani zaidi.
Fedha ni kitu ambacho kipo tu kwa muda kama mtu aliyekuwa nayo sasa akishindwa kuidhibiti leo, kesho hatakuwa nayo. Suala mtambuka hapa ni je, kwa nini niweke akiba au niwekeze kwa jambo lingine?
Ningependa nizungumzie juu ya njia mbalimbali za kuweka akiba ambapo zikitumika zinaweza kukuletea faida kwa karne hii, japo kiuhalisia kwa Waafrika kuweka fedha ni tatizo sugu kwa walio wengi. Hali kama hii inatokana na uwezo mdogo wa kudhibiti fedha kwa mitindo ya kisasa na kibiashara pia. Elimu juu ya jambo hili haijafika au haijakaa vizuri katika upande wa ubongo iliyo wazi kwa mazingira ya hapa nchini.
Zipo njia ambazo ni nzuri zikitumika kwa kuweka akiba kwa faida zitaongeza maendeleo ya wengi. Njia hizo ni:
1», ni kununua fedha za kigeni. Mara nyingi fedha za kigeni mfano Dola za Marekani, Euro, Pound ya Uingereza na fedha kutoka Bara la Asia kama vile za Saudi Arabia, huwa zinapanda thamani ukilinganisha na za Tanzania.
Mfano, ulinunua Dola moja ya Marekani Novemba, mwaka jana kwa Sh1,300. Mwaka huu unaiuza kwa Sh2,100. Ukipiga hesabu umepata faida ya Sh800. Kama ulinunua Dola 10,000, leo hii ikiziuza una faida ya Sh1 milioni, na kadhalika.
Mtindo wa kununua dola kwanza unapunguza kubeba lundo la fedha nyingi, inakuzuia kuitumia bila sababu, hivyo kuendelea kuwa akiba, kukulinda na kukuwezesha uwe na faida pale mfumuko wa bei unapoongezeka na inaweza kukusaidia iwapo itakulazimu usafiri nje ya nchi. Ukisafiri nje ya nchi itakufanya usitumie fedha nyingi za kununua za kigeni kwa gharama kubwa.
2», ni simu benki. Huu ni mfumo ambao upo sana siku hizi eneo la Afrika Mashariki. Siku hizi kampuni za simu zimewezesha mtu kuweka akiba.
Huduma imeboreshwa zaidi kwa kuweza kuzihamishia kwenye akaunti za benki, kulipia huduma na bidhaa au kuzitoa katika nchi nyingine kulingana na aina ya fedha za eneo husika.
Hii inamuwezesha hata kama mtu akiwa mbali na benki na kuwa na uwezo wa kuokoa muda kwa kutumia pesa alizoweka kwenye simu yake kwa kuzitoa kwa wakala aliye karibu naye.
Vilevile, kwa kutumia simu waweza kuvuta fedha kutoka kwenye akaunti yako ya benki na kuziingiza kwenye simu yako na kuwa huru kuzitoa ili kuzitumia eneo lolote kwa kutumia mawakala.
Siku hizi pia kwa kutumia akiba kwenye simu unaweza kupata huduma nyingine kupitia simu hiyo kama vile kununua umeme, kulipia bili ya maji, matibabu, king’amuzi na hata tiketi za kuingia kwenye michezo ya soka au tamasha. Mtu aweza kudunduliza fedha kidogokidogo kwenye simu yake.
3» kuweka akiba kwa kutumia benki na taasisi nyingine za kifedha. Hii husaidia sana kuhamasisha huduma za kuweka akiba kwa malengo kama vile kumsomesha mtoto au amana.
Uwekaji wa fedha za namna hiyo pia huweza kusaidia kuwa na fedha za kukabili dharura na kuwa na mitaji mikubwa ya kibiashara na hatimaye kuleta maendeleo makubwa yaliyokusudiwa.
4», ni kumkopesha mtu na kurudisha kwa riba. Siku hizi aina hii ya ukopeshaji imeenea sana, hasa mijini na vyuoni. Hii imetokana na watu kuzidi kukua sana kiuelewa, wamebadili mwelekeo kutoka kumkopesha mtu pasipo riba hadi kuwa na faida.
Watu wameerevuka na kufahamu kuwa fedha ya mwezi au wiki hii ni tofauti na ya mwezi au wiki lijalo. Tatizo lililopo ni kwamba hakuna maandishi ya kukopeshana kwa walio wengi kwa sababu za kujali utu. Lakini ukweli ni kwamba wanadamu wengi wana tabia ya kubadilika. Kama huna maandishi ya kukopeshana itakuwa vigumu kupata fedha zako pale anapokuwa si mwaminifu.
5», ni kuwekea bima mali zako na biashara yako. Hii ni njia ambayo ni muhimu sana maana hakuna mtu anayeweza kuzuia majanga ambayo ni ya asili au ya kawaida, hivyo bima hasaidia sana siku ukipata ajali ya biashara kwa kuibiwa au kuungua.
6», ni kununua vitu kama nyumba, ardhi na vifaa vya gharama vyenye kudumu muda mrefu. Hivi waweza kuviuza baadaye kwa bei ya juu.
NB.
Maendeleo ya mtu mmojammoja ni mafanikio ya taifa.
Taifa lenye akiba ya kutosha kwa kawaida linakuwa imara na wananchi wenye akiba kwa njia mbalimbali kama nilivyoorodhesha, ni watu wenye maisha ya uhakika. Dharura zote wanaweza kuzikabili na hapa ndipo pia mitaji mikubwa ya biashara inatokea. Kuweka akiba ni jambo la msingi.
ASANTENI
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni